Kuwa na bajeti ni njia nzuri ya kufuatilia mapato na matumizi yako. Pesa inayopatikana inapogawanywa katika kile kinachotumika na kinachobaki, inakuwa rahisi zaidi kuhakikisha kuwa unachotengeneza kinakidhi mahitaji yako yote.
Katika maisha ya kila siku, jambo moja ambalo hutumia gharama kubwa zaidi ni makazi yaani nyumba. Kipengele hiki kinaathiri bajeti yako kwa kiasi kikubwa. Kulingana na mahali unapoishi, makazi yanaweza kuwa ghali sana, na unaweza kulazimika kufanya kazi ya ziada ili kuishi kulingana na mapato yako au unalazimika kutafuta nyumba ya bei nafuu ya kutosha kukuwezesha kuishi kwa raha ndani ya uwezo wako.
Vipengele vingine muhimu katika bajeti yako ni huduma za lazima, chakula, bidhaa na huduma zisizo za lazima.
Ni muhimu kuelewa hali yako ya mapato ili kuishi maisha yasiyo na mashaka. Hata hivyo, ni muhimu pia kujifunza kupitia mifano halisi ya watu wengine. Kumbuka kuwa mfano wa mwajiriwa tutakaoutumia katika makala haya ni mfano tu na haupaswi kuchukuliwa kama pendekezo la lazima. Ikiwa kuna mambo ambayo ni ya muhimu sana kwako ndiyo yanayopaswa kupewa vipaumbele wakati wa kutengeneza bajeti.
Twende kazi…
Katika muktadha huu, tutatumia mfano wa mfanyakazi anayelipwa mshahara wa Tsh 500,000 kwa mwezi na tuone jinsi bajeti yake inavyopaswa kuwa.
Makato ya Kodi
Kila mtu anapaswa kulipa kodi. Ni takwa la kisheria. Kukwepa kulipa kodi kunaweza kukuingiza matatani, na hata kupelekea kifungo kwa mujibu wa sheria za nchi. Ikiwa umeajiriwa, unakatwa kodi PAYE (Pay As You Earn), pamoja na makato ya NSSF na NHIF yatakuacha na takribani 435,600.
Unaweza kutumia kikokotoo cha TRA PAYE hapa au jumla ya makato hapa ili uweze kuona ni kiasi gani unaondoka nacho.
Akiba
Lengo kuu la kupanga bajeti, zaidi ya kuweza kuishi kulingana na uwezo wako, ni kutimiza malengo yako. Ni muhimu sana kuweka kipaumbele cha kutenga mara kwa mara sehemu ya kipato unachopata kuweza kutimiza ndoto zako.
Pesa hizi zinaweza kuwekwa kwenye akaunti yako ya akiba, zikihifadhi kwa ajili ya nyumba ya ndoto yako, au gari ambalo umekuwa ukitamani kuwa nalo au hata kulipa madeni yako ya nyuma.
Inashauriwa kutenga takriban 20% ya mapato yako ya baada ya kodi. Hii ni kanuni maarufu ya kupanga bajeti inayojulikana kama 50:30:20.
Hii ni sawa na Tsh 87,120. Ikiwa huwezi kutunza kiasi hiki, unaweza kuanza kidogo kidoki kisha ukaanza kukukipandisha kwa kadri unavyozidi kupata uzoefu. Lakini ni vizuri kuendelea kujiongeza mwenyewe.
Zaidi ya hayo, hakikisha kwamba unafanya malipo ya madeni (kama unayo) katika utaratibu uliojiwekea. Madeni kama vile mikopo ya HELBS, kulingana na kiasi kilichokubaliwa kwa malipo ya kawaida ya kila mwezi, yanapaswa kuwa katika ile 20% ya mapato yako ambayo yanawekwa kwa ajili ya akiba. Kinachobaki kinaweza kuweka katika mfuko maalum wa dharura.
Kiasi kilichosalia sasa ni Tsh 348,480.
Mahitaji ya Lazima
Kanuni ya bajeti ya 50:30:20 inaelekeza kwamba 50% ya mapato yako baada ya kodi itumike kwa ajili ya mahitaji. Hivi ni vitu ambayo huwezi kuishi bila kuwa navyo a.k.a. mahitaji ya lazima.
1: Nyumba
Nyumba, kwa sehemu kubwa, itakuwa ni hitaji lako muhimu zaidi. Gharama za nyumba zinatofautiana kwa kiasi kikubwa kulingana na mahali unapoishi, aina ya nyumba, ikiwa una-share na wenzako au unaishi peke yako, n.k.
Kwa mfano huu, tuchukue gharama ya nyumba ni sawa na 30% ya mapato yako ya baada ya kodi. Hii ni kanuni ya dole gumba ambayo mara nyingi hupendekezwa – lakini kama unaweza kutumia pungufu ya hapo, itakuwa bora zaidi. Hii ni sawa na Tsh130,680 kwa mwezi. Kwa lugha nyingine ni kwamba, kama mshara wako ni Tsh 500,000, hupaswi kuishi katika nyumba unayolipia zaidi ya Sh 130,680 kwa mwezi.
Kiasi kilichosalia baada ya nyumba sasa ni Tsh 217,800
2: Huduma
Jambo linalofuata kwenye orodha yetu ya Mahitaji ni huduma. Mahitaji haya ni kama vile umeme, gesi ya kupikia na maji. Ikiwa baadhi ya bili hizi huenda tayari zimejumuishwa katika gharama yako ya makazi, kwa hivyo hakuna haja ya kuzihesabu mara mbili.
Pia gharama hizi zitatofautiana kulingana na eneo na aina ya nyumba unayoishi.
3: Usafiri
Hii inaweza kujumuisha mafuta ya gari (kama unalo), nauli za usafiri wa umma, teksi, n.k. Chombo chochote kinachokusogeza kutoka sehemu A hadi B. Tena hii itategemea na mahala unapoishi na jinsi mizunguko yako ilivyo.
4: Chakula
Unaweza kupunguza gharama za matumizi ya chakula ya kila mwezi endapo utaamua kutengeneza chakula chako mwenyewe.
Kwa kufuata kanuni ya 50:30:20, katika bajeti ya Tsh 500,000, mahitaji yako ya lazima hayapaswi kuzidi Tsh 152,460. Huku kodi ikikugharimu Tsh 130,680 na mahitaji mengine yote yanahitaji kutoshea kati ya Tsh 65,340 iliyosalia.
Mahitaji Yasiyo ya Lazima
Kanuni ya upangaji bajeti ya 50:30:20 inapendekeza kwamba ni 30% tu ya mapato baada ya kodi hutumiwa kwa mahitaji yasiyo ya lazima. Hii ni pamoja na vitu kama vile nguo, viatu, burudani, likizo, n.k.
Katika hatua hii, utajaribiwa kutaka kutumia pesa hizi zote. Lakini tena, jaribu kadiri uwezavyo kuwa na mazoea ya kuweka akiba ya pesa taslimu mara kwa mara kwa malengo yako ya baadaye, au hata mfuko wa dharura.
Hata ikikubidi kuanza kidogo kidogo na kuendelea kutokea hapo. Sio lazima utumie yote kwa vitu visivyo vya lazima. Hifadhi zingine zaidi.
Kwa mshahara wa 500k, ukitumia kanuni hii, una takriban Tsh 65,340 za kutumia kununua vitu visivyo vya lazima – mfano kudunduliza kwa ajili ya kununulia kabati la nguo, vyombo, viatu vipya n.k.
Tena, ukiweza kutumia kanuni hili kama ilivyo hainishwa katika mwongozo huu, unaweza kuona kwamba kwenye mshahara wa 500k, endapo utajinyima vitu vya ziada, unaweza kabisa kuokoa takriban Tsh 50,000 kila mwezi ambayo ni takriban Tsh 600,000 kwa mwaka.
Kama u-mwanachama wa SCCF na fedha hizi unaziweka kwenye akiba yako… baada ya mwaka wa kwanza, unaweza kupata mkopo wa riba nafuu ambao ni mara tatu yake, yaani TSh 1,800,000 na ukaweza kuanzisha biashara ndogo na ukazidi kuikuza.
Kumbuka kwamba unapaswa kuwajibika kwa majukumu yako mengine ya kawaida ikiwa ni pamoja na familia, jamii, zaka n.k.
Hitimisho
Kupanga bajeti ni zana nzuri ya kifedha ya kibinafsi, na kila moja ni muhimu kwa muhusika. Unapopitia mchakato wa kupanga bajeti, unapata picha bora ya jinsi unavyoweza kuishi, kwa raha, ndani ya uwezo wako, na zaidi kufikia malengo yako ya kwa siku za usoni.